Tuesday, May 28, 2013

Azam TV wafanya kufuru kubwa Simba na Yanga


KAMPUNI ya SSB inayomiliki klabu tajiri ya Azam FC ipo mbioni kumwaga zaidi ya sh. 1.5 bilioni kwa timu zote za Ligi Kuu Bara msimu ujao na itarusha laivu mechi zao kupitia televisheni yao.
Lakini habari za ndani zinadai Simba na Yanga zinagoma zikitaka kuongezewa fungu kwa madai kwamba televisheni ya kulipia itakayoanzishwa na Azam itanufaika zaidi.
Azam imekusudia kuchukua tenda ya kuonyesha mechi zote za Ligi Kuu Bara kupitia kituo chake kipya cha televisheni (Azam TV) ambacho kitaanza kazi hivi karibuni na ujenzi wa mitambo hiyo unaendelea katika jengo moja lililopo Barabara ya Mandela, jijini Dar es Salaam.
Habari za uhakika zinasema Azam itauza ving’amuzi na inakusudia kutoa kiasi cha Sh. 100 milioni kwa kila timu kwa timu zote 14 zitakazoshiriki ligi msimu ujao.
Jumatano wiki hii Kamati ya Ligi chini ya Wallace Karia na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) walikutana na klabu za Ligi Kuu kujadili mkataba huo ambao utazipunguzia mzigo klabu ndogo ambazo zimekuwa zikisumbuliwa na ukata kutokana na kutegemea udhamini wa Vodacom pekee.
Karia alisema: “Tulikuwa na kikao na kuna televisheni moja ambayo tunataka kuingia nayo mkataba.”
Habari za ndani zinasema Azam TV wataingia mkataba wa miaka mitano kuanzia Agosti na itakuwa ikirusha pia ligi za nchi nyingine za Afrika kama inavyofanya Supersport ya Afrika Kusini.
Hata hivyo, uliibuka mzozo baada ya Simba na Yanga kutaka kupewa mgao mkubwa tofauti na klabu nyingine. Lakini hatma itajulikana wiki ijayo baada ya klabu hizo kukutana tena kujadili mkataba huo, ule wa Supersport pamoja na Vodacom.
Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage alisema; “Hata Manchester United udhamini wake wa Ligi haulingani na Wigan wala Sunderland, wa Man United upo juu kwa vile ni klabu kubwa, sasa iweje sisi tupate sawa na timu nyingine?
“Pili tunataka kuja na mkakati wa kuhakikisha msimu ujao mechi ambazo tutaenda kuzichezea mikoani tunawaachia mapato yote na wao wakija Dar es Salaam mapato ya huku hayawahusu, na huu ni utaratibu wa kawaida tu unaofanyika hata kwenye nchi nyingine, haiwezekani tunatumia shilingi bilioni 2.3 msimu mzima halafu mapato tunayopata ni kiduchu,”alisisitiza Rage.

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home